Gilbert Paul na msalaba uliozua gumzo
Na Charles Kayoka
Wasanii wanasifika sana kwa tabia yao ya kuvunja miiko ya jamii. Ni jambo la kawaida kushudia wasanii wakivaa nguo kinyume na maadili; wasanii wanaume, kwa mfano, wakisuka nywele; wanawake wakivaa vichupi kinyume na walivyolelewa. Lakini pia katika mambo wayafanyayo wasanii pia kwa kutumia lugha, picha au nyimbo, huanzisha mijadala ya wazi ambayo katika hali ya kawaidia si rahisi kuanzishwa kwani watu hudhani mada zinazoibuliwa huwa nyeti. Na mfano mmojawapo ni wa Gilbert Paul (27) aliyeamua kujitengenezea msalaba wake na kuandika tarehe yake ya kuzaliwa na kuweka alama ya kiulizo siku ya kufa kwake.
Mzaliwa wa Namanyere, wilayani Nkansi, Mkoa wa Rukwa, Gilbert anafanyia kazi zake pembeni ya barabara kuu iendayo kituo cha basi mjini Namanyere. Anasema yeye alidhani ingekuwa vizuri watu wakaondoa uwoga kujadili kifo kwani ni kitu ambacho kiko katika hatima ya kila mwanadamu.
“Mimi niliuchora msalaba wangu ili niwaonyeshe wanadamu wenzangu kuwa kifo kinakuja na hakuna sababu ya kugopa,” Gilbert alielezea. Lakini hatua hiyo ya kujiandikia msalaba wake na kuutundika juu ya kibanda anachofanyia kazi zake za kila siku kilimzulia matatizo makubwa.
Kwanza watu walikuwa wakiniogopa. Nikikutana nao njiani wananipisha kwa mbali isivyo kawaida. Nadhani walikuwa wakihisi mimi nilipata kichaa na ningeweza kuwadhuru. Taarifa zingine zinasema walikuwa wakimdai au tayari kumpatia kazi walikuja kumdai au kuondoa oda zao za kuchorewa wakihisi labda angekufa kweli au ameshakuwa kichaa. Lakini yeye mwenyewe alithibitisha kuwa tangu alipojichorea bango lile mwaka 2007, alikaa kwa muda mrefu, upatao mwaka, bila kupata oda za kazi za uhakika kwa sababu ya kumuogopa.
“Watu wazima waliwa wanakuja hapa bandani kuniuliza sababu ya kujichorea msalaba, na walikwenda kushitaki kwa wazazi wangu kuhusiana na hili jambo, “ alieleza Gilbert.
Yeye ni mkristo wa Madhehebu ya Katoliki wa Roma. Anasema baada ya kuchora huo msalaba wa kuzikia Padre mmoja wa hapo parishi yake Namanyele alikuja kumtembelea na moja ya maswali aliyomuuliza ni kama angependa kuzikiwa na msalaba ule. Yeye alitueleza kuwa ingekuwa vyema msalaba huo kama ungetumika lakini wasiwasi wake ni kuwa ungekuwa mpana sana na ungechukua sehemu kubwa.
“Mimi naona kama nimerahisisha kazi kwani siku nikifa kazi inakua kukifuta kiulizo na kujaza tarehe ya kufa kwangu,” alisema.
Lakini kuna wanajesha ambao walimsifia sana, kwa maelezo yake, kwa kufanya uamuzi ule. Huenda kwa sababu wanajeshi ni watu waliojitolea kufa na kuwa kifo ni sehemu ya maisha yao, hasa wanapokuwa msitari wa mbele. Kwa hiyo hawawezi kuogopa kifo wala kushangaa kuona mtu amejiandalia msalaba wake. Lakini pia tunafahamu kuwa jamii nyingi duniani zilikuwa zikijiandalia makaburi, kutoa husia wa namna ya kuzikwa na mahali pa kuzikwa, walijiandalia sana na mengine mengi. Mbona leo tunaogopa! Nini kinatufanya kuogopa kifo na kukwepa kujiandaa.
Ni mawazo yangu kuwa wasanii, kama sehemu muhimu ya jamii, wanaweza kuleta mabadiliko kama wataaibua ajenda ya mambo yanayosaidikiwa kuwa nyeti lakini yana athari kubwa kwa maisha ya jamii. Hiyo ndiyo nguvu ya usanii, kwenda hatua nyingi mbele na kujenga uwelekeo kwa wanajamii yake. Gilbert Paul alizua mjadala pale Namanyere. “na hata sasa hivi naitwa Bwana Msalaba. Mtu akichukua namba yangu ya simu, badala ya kuandika jina langu halisi, anaandika Bwana Msalaba.”