Saturday, September 24, 2011

Fine art

Gilbert Paul na msalaba uliozua gumzo

Na Charles Kayoka

Wasanii wanasifika sana kwa tabia yao ya kuvunja miiko ya jamii. Ni jambo la kawaida kushudia wasanii wakivaa nguo kinyume na maadili; wasanii wanaume, kwa mfano, wakisuka nywele; wanawake wakivaa vichupi kinyume na walivyolelewa. Lakini pia katika mambo wayafanyayo wasanii pia kwa kutumia lugha, picha au nyimbo, huanzisha mijadala ya wazi ambayo katika hali ya kawaidia si rahisi kuanzishwa kwani watu hudhani mada zinazoibuliwa huwa nyeti. Na mfano mmojawapo ni wa Gilbert Paul (27) aliyeamua kujitengenezea msalaba wake na kuandika tarehe yake ya kuzaliwa na kuweka alama ya kiulizo siku ya kufa kwake.

Mzaliwa wa Namanyere, wilayani Nkansi, Mkoa wa Rukwa, Gilbert anafanyia kazi zake pembeni ya barabara kuu iendayo kituo cha basi mjini Namanyere. Anasema yeye alidhani  ingekuwa vizuri watu wakaondoa uwoga kujadili kifo kwani ni kitu ambacho kiko katika hatima ya kila mwanadamu.

“Mimi niliuchora msalaba wangu ili niwaonyeshe wanadamu wenzangu kuwa kifo kinakuja na hakuna sababu ya kugopa,” Gilbert alielezea. Lakini hatua hiyo ya kujiandikia msalaba wake na kuutundika juu ya kibanda anachofanyia kazi zake za kila siku kilimzulia matatizo makubwa.

Kwanza watu walikuwa wakiniogopa. Nikikutana nao njiani wananipisha kwa mbali isivyo kawaida. Nadhani walikuwa wakihisi mimi nilipata kichaa na ningeweza kuwadhuru. Taarifa zingine zinasema walikuwa wakimdai au tayari kumpatia kazi walikuja kumdai au kuondoa oda zao za kuchorewa wakihisi labda angekufa kweli au ameshakuwa kichaa. Lakini yeye mwenyewe alithibitisha kuwa tangu alipojichorea bango lile mwaka 2007, alikaa kwa muda mrefu, upatao mwaka, bila kupata oda za kazi za uhakika kwa sababu ya kumuogopa.

 “Watu wazima waliwa wanakuja hapa bandani kuniuliza sababu ya kujichorea msalaba, na walikwenda kushitaki kwa wazazi wangu kuhusiana na hili jambo, “ alieleza Gilbert.

Yeye ni mkristo wa Madhehebu ya Katoliki wa Roma. Anasema baada ya kuchora huo msalaba wa kuzikia Padre mmoja wa hapo parishi yake Namanyele alikuja kumtembelea  na moja ya maswali aliyomuuliza ni kama angependa kuzikiwa na msalaba ule. Yeye alitueleza kuwa ingekuwa vyema msalaba huo kama ungetumika lakini wasiwasi wake ni kuwa ungekuwa mpana sana na ungechukua sehemu kubwa.

“Mimi naona kama nimerahisisha kazi kwani siku nikifa kazi inakua kukifuta kiulizo na kujaza tarehe ya kufa kwangu,” alisema.

Lakini kuna wanajesha ambao walimsifia sana, kwa maelezo yake, kwa kufanya uamuzi ule. Huenda kwa sababu wanajeshi ni watu waliojitolea kufa na kuwa kifo ni sehemu ya maisha yao, hasa wanapokuwa msitari wa mbele. Kwa hiyo hawawezi kuogopa kifo wala kushangaa kuona mtu amejiandalia msalaba wake. Lakini pia tunafahamu kuwa jamii nyingi duniani zilikuwa zikijiandalia makaburi, kutoa husia wa namna  ya kuzikwa na mahali pa kuzikwa, walijiandalia sana na mengine mengi. Mbona leo tunaogopa! Nini kinatufanya kuogopa kifo na kukwepa kujiandaa.

Ni mawazo yangu kuwa wasanii, kama sehemu muhimu ya jamii, wanaweza kuleta mabadiliko kama wataaibua ajenda ya mambo yanayosaidikiwa kuwa nyeti lakini yana athari kubwa kwa maisha ya jamii. Hiyo ndiyo nguvu ya usanii, kwenda hatua nyingi mbele na kujenga uwelekeo kwa wanajamii yake. Gilbert Paul alizua mjadala pale Namanyere. “na hata sasa hivi naitwa Bwana Msalaba. Mtu akichukua namba yangu ya simu, badala ya kuandika jina langu halisi, anaandika Bwana Msalaba.”



Mlimani City

Mlimani City: Mabadiliko katika utamaduni pendwa

Na Charles Kayoka

Kila ninapofika Mlimani City, moja ya vitu ninavyovibaini ni mabadiliko ya tabia na utamaduni miongoni mwa wakazi wa jiji wanaotumia mahali hapo kukidhi haja mbalimbali, lakini pia unaweza kuona athari katika tabia za kibiashara kwa wajasiria mali hasa huko mitaani.

Kuna ndugu mmoja aliwahi kumaka kuwa anapoaangalia wanaotembelea Mlimani City hujipamba vilivyo na kama hupafanya ndio mahali pa kukutania ndugu na marafiki na hata wenye mipango ya maendeleo. Lakini kwa bahati nzuri, tofauti na maeneo mengine ambayo hutumiwa kwa burudani na kukatana, gharama za viingilio huwa vizuizi kwa kituo hiki cha biashara kipingamizi hiki hakipo. Waweza kuja tu kushangaa shangaa na kuondoka. Ila kwa kweli unapoangalia tabia za watu unaona kama vile ni sehemu za kuonyesha wewe ni nani!  Inakuwa kama vile wanapotaka kufika hapo unatakiwa kujiweka katika hali ya kisasa kwani unaonekana kwa wengi.

Mlimani City pamekuwa eneo lenye uzito wa pekee kwa wanunuzi ambao wamejenga imani kuwa vitu vya hapo ni bora na pengine kusema kuwa ukinunua hapo, na sio pengine, basi wewe ni mtu wa kisasa uendaye na wakati. Hii ni tabia ya walaji, huwezi kuzuia, nap engine miundo mbinu ya mfano huu ilihitajika kuwapo kwa muda mrefu lakini wawekezaji wa ndani hawakuweza kugundua umuhimu wake. Na wachache walioanzisha huduma ya supamaketi kama hizo hawakuweza kupanua dhana ili kutambua kuwa watu wanahitaji sio tu kununua, bali pia kuburudika na kujijengea haiba mpya kama sehemu ya utamaduni pendwa.

Sina ushahidi wa kisayansi katika hili lakini uchunguzi unaonyesha jinsi Mlimani City ilivyoathiri na inavyoweza kuathiri ubora wa huduma za maduka. Ghafula naona kumezuka maduka mengi madogo madogo yanayotaka kutoa huduma za upatikanaji  wakila aina ya bidhaa mahali pamoja, huku wateja wakiruhusiwa kuingia hadi ndani ya duka na kujibebea watakacho kukikunua.

Mlimani City, kwa wale wanaotembea nje ya nchi, wanaweza kusema ni mwelekeo mzuri wa kuwapatia Watanzania huduma bora na za uhakika. Na kuwa licha ya kuwa imechelewa kufika, inahitajika miji mikubwa yote nchini kwa ajili ya kutumika kama kitu cha kusukuma tabia mpya za ujasiriamali, hasa katika sekta ya biashara kwa ujumla. Ukifika mikoani, na Dar-es-Salaam bado ikiwemo, mtu mgeni unapata dhiki sana kutafuta bidhaa katika mfumo wa biashara ambapo unakulazimisha kutembea huko na huko kama unavyovitafuta huwezi kuvipata mahali pamoja.

Mlimani City inatuonyesha uwezekano wa watu wa mipango miji kujenga mfumo wa maduka ambapo maduka yote yanapatikana mahala pamoja na mteja akifika hapo anapata kila aina ya mahitaji yake bila kulazimika kuzurura huko na huko. Miji kam Johannesburg wamejenga mifumo kama hiyo na wateja wanajua kuwa  niendapo kufanya manunuzi sina sababu ya kuhangaika huko na huko kama ilivyo sasa hapa jijini kwetu ambako duka moja la spea liko Tandika, jingine liko Magomeni, na jingine katikati ya jiji. Foleni za magari zinakuwa kubwa bila sababu na gharama za usafiri zinakuwa kubwa vilevile. Mji kama wa Dar-es-Salaam, unahitaji maduka mawili mengine kama Mlimani City ili kutowalazimisha watu wa Temeke, kwa mfano kuja huku Chuo Kikuu, na pia Tegeta, eneo linaloweza kuhudumia watu watokao Bagamoyo pia. Kwa sasa hivi Mlimani City inatoa huduma chache sana na katika eneo dogo kabisa. Unatamani kuwa na duka kubwa kuliko hili, kama ilivyo miji ya wenzetu, ambako unaweza kuingia humo na kushinda mchana kutwa ukifanya manunuzi yako na ukitoka hapo huhitaji kwenda sehemu ingine tena. Na hili lingepunguza utitiri wa maduka ambayo mengi hayana faida kwa wenye nayo na sio hata rahisi kwa mamlaka ya mapato kudhibiti kodi kwa ajili ya mapato ya serikali.

Lakini ni kwa kiasi gani mahala hapo panatumika kufaidisha wakulima na wazalishaji wa aina ingine ndio moja ya maswali ya msingi. Je tunatumiaje miundo mbinu kama hiyo kuwapatia wazalishaji wa ndani soko na pia, kupitia huduma za ugani na ubora wa uzalishaji bidhaa, kuhakikisha kuwa kinachoweza kufika hapo kinakuwa na viwango vya kimataifa. Mlimani City panatumikaje kuinua ubora wa bidhaa za wazalishaji wa ndani? Au ni mahali tu ambapo watu wanakuja kushangaa na kununua bidhaa za nje? Nawapongeza waliobuni wazo la Mlimani City, lakini nataka kuwaambia serikali kuwa hiyo iwe changamoto kwa wajasiriamali wa ndani na sio kutumika kwa ajili kujiburudisha na kununua bidhaa za nje tu.


Witchcraft and Local Faith system- Tanzania

This is a story of a a great witch who was also a seer. he was able to turn his animals into rocks when he dreams that rustlers were about to come
Sitta Gabu: Aliyesifika kwa Utabiri, Uganga!

Na Charles Kayoka

Nikiwa Bariadi hivi karibuni nikifuatilia nyayo na vituko vya Ng’wanamalundi,( nawashukuru wasomaji walionichagiza kufanya utafiti zaidi na kunieleza wapi pa kwenda,) nikakutana na babu mmoja aliyeniambia kuwa eneo moja linaloitwa Kilulu, kilomita kama tano kutoka Bariadi mjini, kuna eneo la mawe ambako aliwahi kusihi mti anayeitwa Sitta, asili ya kabila la Taturu, ambaye alikuwa bingwa wa kutabiri na uganga pia.

Huyu bwana alikuwa na vituko. Kwa maelezo ya wenyeji taarifa zake ni kuwa alikuwa ana uwezo wa kujua nini kitatokea pale kijijini, au kwa mtu binafsi ambaye atafika kuomba msaada wake. Nilipomuuliza mzee huyu kama huo sio ushirikina alikana kwa nguvu na kusema mtu anakuwa mshirikina kama anaroga watu, sasa kama huyu anatusaidia kujua ya mbeleni na kututibu maradhi ushirikina unatoka wapi. Aidha alisema kuwa kosa kubwa lililofanyika ni kuwa Waafrika hatuwa na elimu  na ufahamu wa kuweka kumbukumbu mambo muhimu ya utamaduni wetu.

Wengi wa wenyeji wenye umri zaidi ya miaka hamsini au hata baba zao, hawajawahi kumuona, ila wanajua kuwa aliishi na alama ya kuishi kwake eneo hilo zipo. Tulipofika eneo husika Bibi mmoja wa miaka 60 alikubali kutuongoza katika ziara ile. Alisema kwanza kuwa huyu bwana Sitta alikuwa na uwezo mkubwa wa kufanya maajabu.

Kwanza alikuwa kiboko ya Wamaasai waiba ng’ombe. Alipojiwa na taarifa (ndoto) kuwa kutatokea uvamivi wa waiba ng’ombe aliwabadilisha wanyama wake kuwa mawe. Tulipofika eneo hilo tukafikishwa kwenye nyumba ya mmoja wa waganga anaye endelea kuishi hapo (ni kaya pekee iliyopo neo hilo). Mtoto wake akatupeleka eneo ambalo kuna jiwe lenye mfano wa ng’ombe. Alisema taarifa za Sita zimesafiri katika vichwa vya watu kwa muda mrefu hata ukweli kamili sasa si rahisi kuupata. Alisema ni kweli alikuwa anabadilisha ng’ombe na mbuzi kuwa mawe lakini ushahidi pekee ni hilo jiwe, inawezekana kuwa mawe mengi ya pale ni sehemu ya wanyama aliwabadilisha kabla ya kufa kwake.

Bibi aliyetusindikiza alisema nay eye aliliona jiwe lile kwa mara ya kwanza siku ile ingawa habari zake alikuwa akizisikia tangu alipokuwa mdogo, na visa vya Sita Gabu anavijua. Tukapelekwa eneo la kaburi lake, limefukiwa kwa alama yam awe mengi na pembeni kulikuwa na jiwe lililoandikwa karibu kwa Sitta Gabu. Eneo hilopalikuwa na nyumba yake lakini sasa hakuna hata dalili. (inasemekana aliishi karne ya kumi na tisa mwishoni kuelekea mwanzo wa karne ya ishirini). Eneo hilo tukakuta vibuyu na majivu, ishara ya kuwa matambiko yanaendelea kufanyika kwa kufuata imani juu ya huyu bwana.

Baadaye tukaonyeshwa eneo ki mlima cha mawe kilicho na wastani wa urefu wa mita hamsini hivi. Tukaambiwa kuwa siku zingine Sita alikuwa akipanda kule kwenye kilele cha kilima na kigoda chake na kukaa huko yeye na mkewe wakichunga ng’ombe zake. Namna gani alipanda hakuna anayeweza kujua lakini tulionyeshwa alama ya ngazi ambayo kwa kweli huwezi kupanda. Na kule kwenye kile alitoboa matundu mawili ya kuwekea miguu yake ili isining’inie wakati anapumzika. Na chini yam lima huo kulikuwa na jiwe ambalo lina ishara ya simba. Lakini kutokana na wingi wa umri na kuharibiwa na mvua na upepo, huwezi tena kuitambua kwa urahisi. Chini pembeni yam lima huo kuna bao la jiwe kubwa kwa ajili ya mchezo wa solo. Kuwa alikuwa akija na marafiki zake kucheza solo kwenye jiwe lile. Na mbali na hapo kuna kisima ambacho maji yake hutoweka na kisima kukauka kama wewe ni mtu mwenye nia mbaya. Hatukufika kwa sababu usiku ulishafika tulipaswa kuondoka. Linguine ni kuwa kabla yay eye na mkewe kufa alitengeneza sanamu yake na mkewe kwenye jiwe kubwa. Nayo inapotea kutokana na uchakavu wa jiwe lile ambalo sio gumu sana. Mama mmoja anasema alipokuwa mdogo yeye na wanafunzi wenzake walikuwa wanakuja eneo hilo kushuhudia maajabu ya Sitta Gabu. Lakini kutokana na kutotunzwa mvua, upepo, mchanga na mifumo mingine ya hali ya hewa inapachakaza mahali hapa. Kwani hata hilo bao limebaki vialama tu. Lakini ni ushahidi kuwa karne za huko nyuma watu walikuwa wakishindana kwa uwezo wa uganga na ulozi.

pix. i. The rock on which the great witch, Gabu Sitta was Sitting overlooking his flock of animals.

 The burial place of Gabu Sita. Now a witcraft shrine. Burried 100 years ago