Saturday, September 24, 2011

Mlimani City

Mlimani City: Mabadiliko katika utamaduni pendwa

Na Charles Kayoka

Kila ninapofika Mlimani City, moja ya vitu ninavyovibaini ni mabadiliko ya tabia na utamaduni miongoni mwa wakazi wa jiji wanaotumia mahali hapo kukidhi haja mbalimbali, lakini pia unaweza kuona athari katika tabia za kibiashara kwa wajasiria mali hasa huko mitaani.

Kuna ndugu mmoja aliwahi kumaka kuwa anapoaangalia wanaotembelea Mlimani City hujipamba vilivyo na kama hupafanya ndio mahali pa kukutania ndugu na marafiki na hata wenye mipango ya maendeleo. Lakini kwa bahati nzuri, tofauti na maeneo mengine ambayo hutumiwa kwa burudani na kukatana, gharama za viingilio huwa vizuizi kwa kituo hiki cha biashara kipingamizi hiki hakipo. Waweza kuja tu kushangaa shangaa na kuondoka. Ila kwa kweli unapoangalia tabia za watu unaona kama vile ni sehemu za kuonyesha wewe ni nani!  Inakuwa kama vile wanapotaka kufika hapo unatakiwa kujiweka katika hali ya kisasa kwani unaonekana kwa wengi.

Mlimani City pamekuwa eneo lenye uzito wa pekee kwa wanunuzi ambao wamejenga imani kuwa vitu vya hapo ni bora na pengine kusema kuwa ukinunua hapo, na sio pengine, basi wewe ni mtu wa kisasa uendaye na wakati. Hii ni tabia ya walaji, huwezi kuzuia, nap engine miundo mbinu ya mfano huu ilihitajika kuwapo kwa muda mrefu lakini wawekezaji wa ndani hawakuweza kugundua umuhimu wake. Na wachache walioanzisha huduma ya supamaketi kama hizo hawakuweza kupanua dhana ili kutambua kuwa watu wanahitaji sio tu kununua, bali pia kuburudika na kujijengea haiba mpya kama sehemu ya utamaduni pendwa.

Sina ushahidi wa kisayansi katika hili lakini uchunguzi unaonyesha jinsi Mlimani City ilivyoathiri na inavyoweza kuathiri ubora wa huduma za maduka. Ghafula naona kumezuka maduka mengi madogo madogo yanayotaka kutoa huduma za upatikanaji  wakila aina ya bidhaa mahali pamoja, huku wateja wakiruhusiwa kuingia hadi ndani ya duka na kujibebea watakacho kukikunua.

Mlimani City, kwa wale wanaotembea nje ya nchi, wanaweza kusema ni mwelekeo mzuri wa kuwapatia Watanzania huduma bora na za uhakika. Na kuwa licha ya kuwa imechelewa kufika, inahitajika miji mikubwa yote nchini kwa ajili ya kutumika kama kitu cha kusukuma tabia mpya za ujasiriamali, hasa katika sekta ya biashara kwa ujumla. Ukifika mikoani, na Dar-es-Salaam bado ikiwemo, mtu mgeni unapata dhiki sana kutafuta bidhaa katika mfumo wa biashara ambapo unakulazimisha kutembea huko na huko kama unavyovitafuta huwezi kuvipata mahali pamoja.

Mlimani City inatuonyesha uwezekano wa watu wa mipango miji kujenga mfumo wa maduka ambapo maduka yote yanapatikana mahala pamoja na mteja akifika hapo anapata kila aina ya mahitaji yake bila kulazimika kuzurura huko na huko. Miji kam Johannesburg wamejenga mifumo kama hiyo na wateja wanajua kuwa  niendapo kufanya manunuzi sina sababu ya kuhangaika huko na huko kama ilivyo sasa hapa jijini kwetu ambako duka moja la spea liko Tandika, jingine liko Magomeni, na jingine katikati ya jiji. Foleni za magari zinakuwa kubwa bila sababu na gharama za usafiri zinakuwa kubwa vilevile. Mji kama wa Dar-es-Salaam, unahitaji maduka mawili mengine kama Mlimani City ili kutowalazimisha watu wa Temeke, kwa mfano kuja huku Chuo Kikuu, na pia Tegeta, eneo linaloweza kuhudumia watu watokao Bagamoyo pia. Kwa sasa hivi Mlimani City inatoa huduma chache sana na katika eneo dogo kabisa. Unatamani kuwa na duka kubwa kuliko hili, kama ilivyo miji ya wenzetu, ambako unaweza kuingia humo na kushinda mchana kutwa ukifanya manunuzi yako na ukitoka hapo huhitaji kwenda sehemu ingine tena. Na hili lingepunguza utitiri wa maduka ambayo mengi hayana faida kwa wenye nayo na sio hata rahisi kwa mamlaka ya mapato kudhibiti kodi kwa ajili ya mapato ya serikali.

Lakini ni kwa kiasi gani mahala hapo panatumika kufaidisha wakulima na wazalishaji wa aina ingine ndio moja ya maswali ya msingi. Je tunatumiaje miundo mbinu kama hiyo kuwapatia wazalishaji wa ndani soko na pia, kupitia huduma za ugani na ubora wa uzalishaji bidhaa, kuhakikisha kuwa kinachoweza kufika hapo kinakuwa na viwango vya kimataifa. Mlimani City panatumikaje kuinua ubora wa bidhaa za wazalishaji wa ndani? Au ni mahali tu ambapo watu wanakuja kushangaa na kununua bidhaa za nje? Nawapongeza waliobuni wazo la Mlimani City, lakini nataka kuwaambia serikali kuwa hiyo iwe changamoto kwa wajasiriamali wa ndani na sio kutumika kwa ajili kujiburudisha na kununua bidhaa za nje tu.


No comments:

Post a Comment